Serikali kuweka ruzuku ya bilioni 150 kwenye mbolea

0
239

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 iliyowasilishwa bungeni hapo jana na Waziri Hussein Bashe na kujadiliwa na Wabunge mbalimbali.

Akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia bajeti hiyo, Waziri Bashe amesema Serikali itatoa shilingi bilioni 150 ili ziwekwe kwenye mbolea kama ruzuku, lengo likiwa ni kunusuru wakulima na upandaji wa bei ya mbolea nchini.

Amewashauri wabunge kutofanya siasa kwenye suala la kilimo na ni muhimu wakatambua kuwa bei za mbolea zipo wazi na serikali inatoa ruzuku ili kuboresha sekta hiyo.

Kuhusu ubadhirifu wa fedha za ushirika, Waziri Bashe amesema kamwe serikali haitawavumilia watu wanaofanya ubadhirifu huo na badala yake itawashughulikia.

Pia amesisitiza kuwa serikali haitafanya kazi na benki zitakazoshindwa kutoa mikopo kwa mfumo wa tarakimu moja.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 wizara ya Kilimo imeomba kupatiwa shilingi bilioni 751 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo.