Dakika 90 za Aprili 30 ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa zilimalizika kwa timu zote kugawana alama moja moja katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini sasa mbabe lazima apatikane katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Mchezo huo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam utaikutanisha miamba ya soka nchini, Simba SC na Yanga SC baada ya timu hizo kuwafungasha virago wapinzani wao katika michezo ya robo fainali.
Yanga ilikuwa ya kwanza kutinga nusu fainali baada ya kuiondoa Geita Gold FC, wakati Simba SC imewaondoa wakulima Pamba SC.
Katika mchezo mwingine wa nusu fainali, Azam FC itakutana na Coastal Union baada ya timu hizo kuzitoa Polisi Tanzania na Kagera Sugar FC, mtawalia.
Simba ndiye bingwa mtetezi wa kombe hilo baada ya kuifunga Yanga SC katika mchezo uliofapigwa kwenye dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma mwezi Julai mwaka jana.