Wanaume wajitokeza kupinga unyanyasaji

0
180

Imeelezwa kuwa jamii imeongeza kiwango cha uelewa juu ya kuripoti masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye familia, ukiwemo unyanyasaji wa wanaume unaofanywa na watu wao wa karibu.

Hayo yameelezwa na afisa wa dawati la jinsia na watoto mkoani Arusha, Happy Mshana kando ya mafunzo yanayoshirikisha maafisa ustawi wa Jamii, wahudumu wa afya na azaki zianazotoa huduma ya afya ya jamii mkoani humo yaliyoandaliwa na taasisi ya PHEDES Tanzania.

Amesema jamii imepata elimu na kwa sasa anapokea kesi nyingi za Wanaume wakidai kunyanyaswa na hivyo kuwapa mbinu za kukabiliana na kadhia hiyo

“Zamani Wanaume walikuwa hawajitokezi kuripoti ukatili wanaofanyiwa kwenye jamii hasa waliokuwa wakinyimwa unyumba na wake zao, lakini sasa hivi Wanaume wanajitokeza wanaripoti na tunawasaidia kupata ufumbuzi wa ukatili wanaofanyiwa, na yanoyokuwa ni ya kiimani zaidi tunawashauri kwenda kwa uongozi wa kidini.” amesema Happy

Kwa upande wake Mkurugenzi wa PHEDES Tanzania, John Ambrose ambaye pia ni mkufunzi wa masuala ya afya ya akili ambao ndio waandaji wa mafunzo hayo amesema, jamii inapaswa kubadili mtazamo juu ya Mwanaume kwani kwa sasa inaaminika mambo maovu yanafanywa na Mwanaume pekee au wakati wa majanga ya magonjwa, moto na majanga mengine Mwanaume anatakiwa kuwa mstari wa mbele.

“Kwa kuliona hili tumeamua kutoa mafunzo hasa kwa wanaotoa huduma ya afya ya akili na saiokolojia ili iweze kuwasaidia Wanaume wote wanaokabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia na kupata ustawi wa maendeleo ya jamii.” na kuongeza kuwa

“Afya ya Akili ndio mpango mzima ambao ndio unaobeba fikra, hisia, na mawazo sahihi kufanya mambo yenye tija kwa jamii.” amesema Ambrose