Video ya wimbo ‘Mtasubiri Sana’ yapigwa stop

0
320

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeviagiza vyombo vyote vya utangazaji na mitandao ya kijamii nchini kutorusha video ya wimbo uitwao ‘Mtasubiri Sana’ ulioimbwa na msanii Nasib Abdul maarufu Diamond Platnumz kwa kushirikiana na Zuhura Othuman Soud maarufu Zuchu, hadi hapo wasanii hao watakaporekebisha sehemu ya video ya wimbo huo ambayo imemeta ukakasi.

Kwa mujibu wa TCRA, katika video ya wimbo huo kuna kipande kimeonesha wahusika wapo kanisani wanaimba kwaya lakini baadae wakaacha na kuelekea kwingine, kitendo kilicholeta ukakasi miongoni mwa waumini wa madhehebu ya dini na kuleta hisia kuwa ni dharau juu ya dini/madhehemu fulani.

Taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Jabiri Bakari imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya TCRA kupokea taarifa kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ya kuzuia usambazaji wa video ya wimbo huo unaopigwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya utangazaji.