Dkt. Ashatu : Upandishaji holela wa bei haukubaliki

0
872

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema kamwe Serikali haitakubali upandaji holela wa bei za bidhaa mbalimbali hapa nchini.h

Dkt. Ashatu ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka fedha wa 2022/2023.

“Upandaji bei holela ambao kamwe haukubaliki ni jinai na Serikali itachukua hatua, sheria zipo za kusimamia biashara na kitendo cha kupandisha bei kiholela bila sababu za msingi ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 9 (1) cha sheria ya ushindani Na. 8 ya 2003.” amesema Dkt. Ashatu

Amesema Serikali itatumia sheria na kanuni zilizopo kudhibiti mwenendo batili wa bei na kwamba kupanga bei, kufanya mgomo, kukubaliana katika manunuzi na kuzuia uzalishaji ni makosa yanayostahili adhabu hivyo wafanyabiashara hawana sababu ya kupandisha bei.

Waziri huyo wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara pia amewaelekeza wauzaji na wasambazaji wa mbolea zenye bei elekezi kuhakikisha wanazingatia bei zilizopangwa na Serikali na watakaokiuka watachukuliwa hatua kali isheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni za biashara.