Coaster kutoa huduma katika matukio muhimu

0
230

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeridhia ombi la kutoa leseni ya utoaji huduma kwa mabasi madogo aina ya Coaster kwa ajili matukio muhimu na ya dharura ndani ya jamii.

Akitoa tamko hilo mkoani Dar es Salaam kwenye majadiliano maalum na wadau wa usafirishaji wa Coaster za kukodi, Mkurugenzi wa barabara kutoka LATRA, Johansen Kahatano amesema wadau hao wanapaswa kuzingatia matakwa yote ya kanuni za mamlaka hiyo.

Kahatano amesema miongoni mwa matakwa ya kikanuni ni pamoja na madereva wanaoendesha magari hayo kusajiliwa na kupata mafunzo na kisha kufanya mitihani ya kuwapima.

Amesema wamiliki wa magari hayo wanatakiwa kufunga kifaa maalum cha kufuatilia mwenendo wa magari hayo ili kubaini hali ya utoaji huduma inavyotendeka.

Kwa mujibu wa Kahatano, magari hayo ambayo mengi yamejikita katika shughuli za kusafirisha harusi, misiba na safari maalum za kukodi ndani ya jamii, hayatakiwi kuingilia na kuathiri utoaji huduma za usafiri kwa watoa huduma wengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa mabasi ya kukodi mkoani Dar es Salaam, Eustack Msoka amesema leseni ya kutoa huduma hiyo ndio iliokuwa kilio chao kikubwa kwa muda mrefu.

Nao Madereva wamesema Wapo tayari kupata mafunzo mapya ya kazi yao Pamoja na kufanya mitihani Ili kuongeza ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto ya barabarani.