Rais Samia: Waandishi wa Afrika msikubali kutumika

0
316

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka waandishi wa Habari wa Bara la Afrika kutokubali kutumika kuvuruga amani na umoja wa nchi zao.

Rais ametoa rai hiyo wakati wa hafla ya kuhutimisha maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani ambayo kwa bara la Afrika imeadhimishwa jijini Arusha, Tanzania.

“Nchi tajiri zinaandika habari za nchi maskini, nchi maskini nazo zinaandika habari za nchi kubwa, lakini uandishi wetu unakuwa tofauti,” maneno ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa waandishi wa habari wa Afrika katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Aidha Rais ameweka msisitizo wa kuwataka waandishi kutokubali kutumika kuichafua Afrika kwani kwa muda mrefu imekuwa ikiandikwa kama bara lenye vita, umaskini na migogoro, habari ambazo zinaandikwa na waandishi kutoka Afrika ili kujipatia fedha.

“Wale wakubwa wanaandika za kwetu kwa kina lakini na vijichumvi kidogo. Lakini habari zile wanapewa na nani? Na ninyi ambao wengine mnajiita mawakala wa vyombo hivyo,” amesema Rais huku akisisitiza kwamba Afrika ni bara bora zaidi ya yote, na ni muhimu waandishi wakausema uzuri huo.

Aidha, ametumia siku hii kuzungumzia mmomonyoko wa maadili unaosababishwa na mitandao ya kijamii, huku akiwataka waandishi kubeba jukumu  la kuwaelimisha wananchi juu ya athari za katuni zisizofaa, uwekaji wa picha za utupu mitandaoni  kwani wengine hufanya hivyo ili wapate fedha na umaarufu.

Amewaahidi waandishi kuwa serikali yake itaendeleza ushirikiano na sekta hiyo, lakini amewataka kuheshimu busara inayotumika wakati huu ambapo sheria na kanuni zinafanyiwa mabadiliko.

“Ukinikuna vizuri, mimi nitakukuna na kukupapasa huku nakupuliza, lakini ukinipara nitakuparura. Twende tufanye kazi kwa ushirikiano,” amesisitiza Rais Samia