Sheikh Mkuu wa Tanzania MUFTI, Abubakar Bin Zuber, amewakumbusha waumini wa Dini ya Kiislam na Watanzania wote kuendelea kujiandaa na zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu.
MUFTI, Zuber ameyasema hayo wakati akitoa Mawaidha katika Swala ya Eid El Fitr iliyofanyika kitaifa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed (VI) BAKWATA Makao Makuu Dar es Salaam, ambapo amewasihi watanzania kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa sensa akieleza faida za sensa ya watu na makazi.
“Sensa ipo na Serikali imetuwekea utaratibu mzuri na sisi viongozi wa Dini tuwe mstari wa mbele kuhamasisha waumini wetu kushiriki kwenye sensa ili watanzania wote tuhesabiwe na kufanikisha lengo la kujua idadi halisi ya Wananchi na makazi”- ameongeza MUFTI.
Aidha MUFTI Zuber amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza filamu ya Royal Tour na kusema filamu hiyo imeitangaza Tanzania ulimwenguni na kuvutia watalii kuja kutembelea vivutio hapa nchini na hivyo Taifa kuingiza Pato na kuzalisha Ajira huku akiwataka watanzania kujivunia filamu hiyo na kuendelea kuitangaza kwa juhudi zote.