Rais Samia: Elimu ya jinsia inatolewa kwa wanaume na wanawake

0
234

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwamba kosa lilifanyika kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake pekee na kuwacha wanaume.

Akizungumza na Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass nchini Marekani, Rais Samia ameeleza kuwa utaratibu wa utoaji elimu kwa sasa unaangazia jinsia zote, kwani vitendo hivyo si vizuri kwa wanaume na wanawake kwa ujumla.

Aidha, ameeleza kutokana na waathirika wengi wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kutofuata utaratibu wa kisheria na kuamua kumalizana na wahusika nje ya mahakama, mkazo zaidi unawekwa kwenye elimu ya kumaliza vitendo hivyo.

Katika kufanikisha hilo ameeleza kuwa serikali inashirikiana na asasi za kiraia kufikisha elimu kwa wananchi wengi zaidi ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikisababisha majeraha, ulemavu na hata vifo.

Kwa upande wake Malpass ameunga mkono utaratibu huo na kuongeza kuwa “wanaume ni sehemu ya tatizo, hivyo wanapaswa kupewa elimu, na kuwekwa mstari wa mbele.”