CCM yasisitiza uboreshaji wa barabara Kigamboni

0
273

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema chama hicho kitaendelea kuweka msukumo kuhakikisha miundombinu ya barabara na vivuko inaboreshwa wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam kwa kuwa wilaya hiyo ni lango la uchumi wa Taifa.

Amesema kwa sasa asilimia 90 ya mafuta yanayotumika nchini yanapitia Kigamboni ambapo magari kutoka mikoa mbalimbali yanafika wilayani humo kuchukua bidhaa hiyo, lakini kumekuwa na changamoto ya kulifikia eneo hilo kiurahisi.

Akizungumza wakati wa muendelezo wa ziara yake wilayani Kigamboni yenye lengo la kufuatilia mchakato wa uchaguzi ngazi ya mashina Chongolo amesema, kutokana na changamoto hiyo CCM itawasiliana na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuangalia namna ya kuboresha miundombinu hiyo.

“Tunaona kasi ya ukuaji wa Kigamboni na magari yamekuwa mengi na yanachukua hadi muda wa masaa matatu kuifikia, naondoka na changamoto hii naenda kuongea na Tanroads na Tarura kuona namna ya kuboresha barabara, kwa kuwa Kigamboni ni lango la uchumi,” amesema Chongolo

Kuhusu changamoto ya vivuko, Chongolo amezitaka Mamlaka husika kutengeneza vivuko vilivyoharibika kwani vivuko hivyo si anasa bali ni huduma.