Mkurugenzi halmashauri ya Mvomero asimamishwa kazi

0
243

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Hassani Njama ili kupisha uchunguzi.
 
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na TAMISEMI imeeleza kuwa Waziri Bashungwa amechukua hatua hiyo baada ya Mkurugenzi huyo kushindwa kutekeleza maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya mwezi Machi mwaka huu kwenye halmashauri hiyo.
 
Wakati wa ziara hiyo Waziri Bashungwa alibaini upotevu wa fedha za miradi na matumizi yasiyo sahihi ya shilingi milioni 231.84 katika ujenzi wa shule ya sekondari ya Kumbukumbu ya Moringe Sokoine zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula.
 
Baada ya kubaini upotevu huo, Waziri Bashungwa alimuagiza Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero  kuwachukulia hatua za kiutumishi wakuu wote wa idara na watumishi waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi katika mradi huo, agizo  ambalo halijatekelezwa mpaka sasa.