Tanzania Royal Tour kuwafikia watu bilioni 1

0
5710

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema wanatarajia kuwafikia watu bilioni moja katika mwaka mmoja kusambaza filamu ya Royal Tour.

Dkt. Abbasi amesema kuwa mikakati mbalimbali imewekwa ya kusambaza filamu hiyo itakayozinduliwa kesho jijini New York, Marekani na kisha Los Angeles, Dar es Salaaam na Zanzibar.

Amesema kuwa itaoneshwa kwenye kumbi za sinema, kwenye ndege, mitandao ya kijamii, yote hayo ikilenga kuwafikia watu wa makundi mbalimbali.

Ameongeza kwamba, akiwa ziarani nchini Marekani, Rais Samia Suluhu Hassan atakutana na makundi mbalimbali ya wasanii na wafanyabiashara ambao watapata wasaa wa kutazama filamu hiyo inayoonesha fursa za uwekezaji na utalii nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana amesema vivutio vingi vya utalii nchini havijulikani, lakini kupitia filamu hiyo vitajulikana na watalii wengi zaidi watafika Tanzania.