Vyombo vya habari vifanye kazi kwa weledi

0
396

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ili kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi, vyombo vya habari havina budi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi pamoja na kutanguliza uzalendo na maslahi ya Taifa.

Pia, Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kusimamia matumizi ya mitandao ya kijamii ili pamoja na kuongeza upatikanaji wa habari kuwepo na uzingatiaji wa maadili na weledi.

Ameyasema hayo jana (Alhamisi, Aprili 14, 2022) wakati akizindua vituo vya Kurushia Matangazo ya Redio vya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Wilayani Ruangwa – Lindi kwa niaba ya vituo vingine vya wilaya za Ludewa (Njombe), Mlimba (Morogoro) na Ngara (Kagera)

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu shilingi milioni 430 kwa udhamini wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Pia vituo vingine vitatu vilivyozinduliwa leo navyo ujenzi wake umedhaminiwa na UCSAF.

Amesema maeneo mengine ambayo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF ni katika wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi), Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Mlele (Katavi), Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro (Arusha).

Naye, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashimba amesema serikali kupitia mfuko huo utaelendelea kuboresha mawasiliano na usikivu wa huduma za radio kwa kuwafikia wananchi kote nchini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Ryoba Chacha amesema, Shirika hilo limejipanga kuhakikisha wanaendelea kuuhabarisha umma wa wa Tanzania kwa uhakika na weledi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi huku akiishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya shirika hilo.