Rais Ramaphosa awakemea wanaowashambulia wageni

0
202

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameyakemea makundi yanayoendesha mashambulio dhidi ya raia wa mataifa ya kigeni nchini humo, na kusema kuwa tabia hiyo haina tofauti na ubaguzi wa rangi unaoendeshwa na watu weusi.

Rais Ramaphosa amesema vitendo hivyo vinapaswa kukemewa kwa nguvu zote, kwani vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi hiyo hasa ikizingatiwa kwamba uchumi wa Afrika Kusini pia unategemea mataifa ya nje.

Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka nchini humo ambapo wiki iliyopita kundi la wananchi raia wa Afrika Kusini lilimshambulia na kisha kumchoma moto raia mmoja wa Zimbabwe, Elvis Nyathi katika kitongoji cha Diepsloot karibu na jiji la Johannesburg.

Rais huyo wa Afrika Kusini amesema vyombo vya usalama nchini humo vitahakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa na wahusika wote wanachukuliwa hatua kali za kisheria.