Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, limemvua
madaraka Meya wa manispaa hiyo Juma Raibu kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia madaraka yake vibaya na kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutoa vibali vya ujenzi katika maeneo kadhaa.
Raibu amevuliwa madaraka baada ya Madiwani 18 kupiga kura za ndio, huku wengine 10 wakipiga kura za hapana wakati wa kutoa uamuzi wa kumvua madaraka Meya huyo.
Akitangaza matokeo ya kura hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Moshi Rashid Gembe amesema, kwa mujibu wa kanuni ya 2 tafsiri ya kanuni ya kudumu ya Manispaa ya Moshi ya mwaka 2015, kwa sasa Baraza hilo litaongozwa na Naibu Meya Stuart Nkinda katika kipindi chote cha mpito.
Aidha kwa mujibu wa Kanuni ya 5(8) aliyekuwa Mstahiki Meya Juma Raibu anaweza kukata rufaa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iwapo hataridhika na uamuzi wa Baraza hilo.