Waziri Nape ziarani kuhamasisha uwekaji wa anwani za makazi

0
255

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ameitaja mikoa ya Tanga na Dar es Salaam kuwa bado haijafanya vizuri katika mfumo wa uwekaji wa anwani za makazi.

Waziri Nape ameyasema hayo mkoani Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya kuondoka mkoani humo kuelekea Tanga, kwa lengo la kuhamasisha uwekaji wa anwani za makazi ambapo pia ataelekea katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Amesema tathmini inaonesha utekelezaji wa uwekaji mfumo huo umefikia asilimia 69, huku baadhi ya maeneo yakikabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Kwa muda uliobaki tumekubaliana tuongeze nguvu kwa kutoka ofisini na kuifikia mikoa yote nchi nzima ili kukagua na kuhamasisha utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi unaojumuisha ukusanyaji wa taarifa, kuweka taarifa kwenye mfumo wa kidijitali na uwekaji wa namba za nyumba, majina ya barabara na mitaa.” Amesema Waziri Nape

Ameongeza kuwa mfumo wa anwani za makazi unalenga kuhakikisha kila Mtanzania anatambulika mahali alipo, mahali anapofanyia kazi, biashara na mahali anapoishi, na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi ambazo mtu anaweza kupata huduma akiwa nyumbani kwake.