Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa moja kati ya mipango yake ni kuirudisha Tanzania kwenye uchumi wa kati pale ilipokuwa awali.
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa mkutano wa kitaifa wa Haki, Amani na Maridhiano na kusisitiza kuwa jambo hilo linawezekana ndani ya kipindi cha miaka miwili.
“Tanzania yetu ilikwenda tukafika uchumi wa kati tukarudishwa, sasa hivi kazi yetu ni kupambana kurudi tulipokuwa,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa;
“Kwa mipango na jinsi ninavyoiendesha Serikali nina imani tutakapofika 2025 kama hatujafika tukakuwa tunakaribia, kwa sababu natarajia mwaka ujao tutakwenda kukua kwa 5% [na] pointi. Miaka miwili inayokuja tutafika kwenye 6.9% tuliyokuwa before [kabla].”
Aidha, Rais Samia amewataka Viongozi wanaoshiriki kwenye mkutano huo wa kitaifa wa Haki, Amani na Maridhiano kuhakikisha wanajadili kwa mapana haki zao na za wengine kwa kuzingatia kuwa haki ya mmoja inapoishia ndipo ya mwingine inaanza.