Rais aagiza kuanzishwa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo

0
248

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara Kilimo ishirikiane na Wizara ya Fedha na Mipango, kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo ambao utachangiwa na tozo maalum kwenye mazao ya kilimo, Mfuko Mkuu wa Serikali na wadau wa maendeleo.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akizindua ugawaji wa vitendea kazi vya maafisa ugani kilimo ikiwemo pikipiki, vifaa vya kupima afya ya udongo, simu janja na visanduku vya ufundi kwenye hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete.

Amesema Mfuko huo utakuwa na majukumu ya kugharamia pembejeo za kilimo kama ilivyofanyika kwenye korosho, pamba na tumbaku ili mfuko huo utumike kama ruzuku pindi pembejeo zinapopanda bei.

Kwa upande mwingine, ameagiza mashamba yote ambayo yapo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kufufuliwa na kuanza kutumika kwa kushirikiana na Sekta binafsi kwa mfumo wa kukodisha ardhi kwa muda mrefu.

Sekta ya kilimo nchini imeendelea kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa taifa ambapo kwa mwaka 2020 sekta ya kilimo ilikua kwa 4.9 %, kuchangia kwa 26.9% katika pato la taifa, kuchangia kwa 61.1% katika kutoa ajira kwa Watanzania na kuchangia kwa 65% ya malighafi za viwandani.