Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, amewaomba viongozi wa dini na waumini kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake ili waweze kuongozwa na hekima ya Mungu katika kuwatumikia wananchi.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Dominika ya 5 ya Kwaresma iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Njombe, Makamu wa Rais amewaomba viongozi wa dini na waumini kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake ili waweze kuongozwa na hekima ya Mungu katika kuwatumikia wananchi. Amewasihi kuendelea kudumisha pamoja na kumuomba mwenyezi Mungu aendelee kuijalia Amani Tanzania.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Njombe na watanzania kwa ujumla kujitokeza katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka hu una kuongeza kuwa zoezi hilo litarahisisha utambuzi wa mahitaji na changamoto zinazowakabili wananchi na kurahisisha mipango ya maendeleo.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo la Njombe, Mhashamu John Ndimbo amemshukuru Makamu wa Rais kwa kushiriki ibada hiyo katika kanisa kuu Njombe na kumuhakikishia kwamba kanisa katoliki kwa miaka mitatu limetoa kipaumbele cha pekee katika uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia umuhimu wake kwa maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameambatana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango katika Ibada hiyo.