Wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekubali ombi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) la kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.
Hatua hiyo imetangazwa leo katika mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao chini ya Mwenyekiti wake Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Akitangaza hatua hiyo Rais Kenyatta amesema ni jambo la kihistoria kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki, na kwamba kukubaliwa kwa DRC kuingia EAC kunaashiria tukio muhimu katika historia ya ushirikiano wa eneo hilo.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inakuwa nchi ya saba mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwezi Februari mwaka 2021, DRC ikiwasilisha ombi EAC la kutaka kujiunga na Jumuiya hiyo.