MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO INAKWENDA VIZURI,RAIS ATOA TATHIMINI

0
159

Rasi Samia Suluhu amesema kuna miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ameipokea na kuhakikisha inaendelea vizuri.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo katika mahojiano maalum na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt.Ayub Rioba Chacha, mahojiano yanayoangazia mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita madarakani.

“Kwanza nimetoa kipaumbele kwa miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea nikahakikisha nakwenda nayo kuitekeleza, na miradi inakwenda vizuri sana.” Rais Samia

Rais Samia ametoa tathmini ya miradi hiyo kama ifuatavyo

RELI YA KISASA

“Reli ya mwendokasi tunayoijenga tunakwenda nayo vizuri, reli inaendelea Mungu ametusaidia kwenye huo mradi hatudaiwi kila wakimaliza kazi wakileta tunalipa, kwa hiyo tunaendelea kutafuta fedha za kumalizia sehemu iliyobaki, nia ni kwenda na reli mpaka Kigoma waunganishe na Burundi na Rwanda na DRC.”

BWAWA LA KUFUA UMEME LA NYERERE

“Mradi wa pili niliyourithi ni mradi wa bwawa la umeme la Nyerere, nilipopokea ilikuwa ni kwenye asilimia 46 ya ujenzi sasa tumeshafika asilimia karibu 57-58, na huu mradi utachelewa ulikuwa umalizike mwaka huu lakini kwa sababu mbalimbali tutamaliza mwaka 2024, tuna delay ya mwaka mzima ila kwa sasa unakwenda vizuri yale ambayo yamesababisha tuchelewe pamoja na UVIKO dunia nzima ilikuwa imesimama na mambo mengine, lakini sasa dunia inafunguka tutaumaliza, kuna changamoto tunazitatua tunakwenda nazo.”

DARAJA LA KIGONGO – BUSISI

“Mradi mwingine ni daraja la Kigongo – Busisi huko Sengerema, Mwanza na lenyewe linakwenda vizuri progress inapatikana, nimepokea kwenye asilimia 20 ya ujenzi sasa tupo 35 -36 tunakwenda vizuri na tutalimaliza kwa wakati

BARABARA

“Kuna Barabara kadha nchi nzima ambazo zilikuwa kwenye ujenzi na ujenzi unaendelea vizuri hakuna madeni hakuna kelele, kelele zetu mkandarasi akizubaa tunakwenda tunasukuma barabara zina endelea

DARAJA LA TANZANITE

“Daraja la Tanzanite la Dar es Salaam tumelimaliza.”

Rais Samia amemaliza kwa kusema “miradi mingi ambayo nimeipokea nimekwenda nayo vizuri lakini tutaleta na mema mapya tunajipanga kuleta mema ambayo mengine tumegusia mengine yatakuja,”

BOMBA LA KUSAFIRISHA MAFUTA GHAFI KUTOKA UGANDA KWENDA TANZANIA

“Tulikuwa kidogo hatuendi vizuri kwenye bomba Uganda, lakini nilivyokwenda tukaelezana twende vipi, vikwazo ni nini kwa upande wetu na kwa upande wao, tumezungumza tumesaini sasa mradi upo karibu kuanza na mwingi upo kwetu kuliko kwao, source ya mafuta ipo kwao lakini ajira na upakiaji mwingi ni kwetu,”