Majaliwa avutiwa na ujenzi wa soko la Machinga

0
3549

Waziri Mikuu Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa sawa ya kufanya biashara katika mazingira bora na rafiki kwa biashara.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipotembelea mradi wa ujenzi wa soko la Wafanyabiashara wadogo (Machinga Complex) lililoko barabara ya Bahi mkoani Dodoma na kueleza kuridhishwa na ujenzi huo.

“Lengo la maboresho haya kwa Wafanyabiashara wadogo ni kutaka kutengeneza fursa zaidi  kwa kuwa na maeneo salama yanayotambulika na yanayoweza kutumika na taasisi za kifedha kutoa mikopo na fursa nyingine za kiuchumi.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Ameupongeza uongozi wa mkoa wa Dodoma kwa ubunifu na kuutaka kuendelee kusimamia mradi huo na kuukamilisha kwa wakati pamoja na kubuni maeneo mengine ya nje ya mji Ili kukuza maeneo mengi zaidi kibiashara katika mkoa huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema, mkoa wa Dodoma umefanya kazi kubwa ya kutekeleza mradi rafiki kwa Wamachinga wa mkoa huo.

“Niwasihi wakuu wa mikoa mingine kuiga mfano huu kwa kujenga miradi ya kuwapanga Wamachinga kulingana na mazingira yaliyo katika mikoa yenu.” ameelekeza Waziri Bashungwa