Jeshi la Russia kusaidia kuondoa Wanafunzi wa Kitanzania Ukraine

0
325

Russia imetengeneza njia salama kuwawezesha Wanafunzi wa Tanzania walioko katika Chuo cha Taifa cha Sumy nchini Ukraine waondoke nchini humo na kwenda Russia na baadaye zifanyike taratibu
za kuwarejesha Tanzania.

Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Tanzania nchini Russia imewataka Wanafunzi hao kuelekea eneo la Sudja ambako watapokelewa na jeshi la Russia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutoka Sudja watasafirishwa na jeshi hilo la Russia hadi eneo la Belgorod ambapo watapokelewa na maofisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Moscow kwa taratibu zingine za kurejea nyumbani Tanzania.

Ubalozi wa Tanzania nchini Russia umewashauri Wanafunzi waliopo katika chuo hicho cha Taifa cha Sumy nchini Ukraine
kutoka chuoni kwa makundi na kubeba bendera ya Tanzania ili kuwatambulisha wanapopita kwenye njia hiyo salama iliyotengenezwa na jeshi la Russia, lengo likiwa ni kurahisisha utaratibu wa mapokezi.