Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Profesa Florens Luoga amesema kuna haja kwa benki za hapa nchini kutoka nje na kwenda kutafuta fursa za kibiashara kwenye mataifa mengine.
Profesa Luoga ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa jengo jipya la makao makuu ya benki ya CRDB ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tanzania imeimarika katika utoaji wa huduma za kifedha ikilinganishwa na nchi nyingi, hivyo ni vema ikatafuta fursa za kibiashara katika nchi hizo.
“Baadhi ya magavana wa nchi jirani wananiomba mabenki yetu kupeleka huduma za kifedha huko, nadhani huu ni wakati wa mabenki yetu kuona haja ya kwenda kuwekeza huko na hii itasaidia Tanzania kujiimarisha zaidi kiuchumi.” amesisiitiza Profesa Luoga