Viwanda Kumi vya dawa vinatarajiwa kujengwa wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni matokeo ya safari ya hivi karibuni ya Rais Samia Suluhu Hassan huko Dubai ambako amefanikiwa kushawishi Wawekezaji kuwekeza Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amosi Makalla mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua jengo jipya la makao makuu ya benki ya CRDB.
Amesema safari ya Rais Dubai imeleta Neema kwa Watanzania na ni fursa kwa wengi, na hivyo kuwataka
Watanzania kuchangamkia miradi mbalimbali pindi itakapoanza kutekelezwa nchini.
“Tunakushukuru Sana Rais Samia maana ziara yako imeleta faida kubwa kwa Taifa hasa baada ya kusainiwa mikataba 36 yenye thamani ya shilingi trilioni 17, niombe tu mabenki yetu yaendeleee kuwawezesha wajasiriamali kupata mikopo Ili wafanye biashara.” ameongeza Makalla
Aidha makalla amesema benki zimeendelea kuimarika kila wakati kutokana na sera nzuri za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuchangia pato la Taifa na Wananchi kwa ujumla.