Ujenzi wa jengo la Ubalozi kuanza Mei

0
1050

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameiagiza wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha ujenzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya na kitega uchumi cha Ubalozi huo unaanza mara moja.
 
 
Dkt.  Mpango ametoa agizo hilo nchini Kenya alipotembelea eneo la Upper Hill lililopo jijini Nairobi ambapo kuna kiwanja kinachotarajiwa kujengwa jengo la ghorofa 23 la Ubalozi wa Tanzania nchini humo pamoja na kitega uchumi cha Ubalozi huo.
 
 
Amesema tayari Serikali imetoa fedha za ujenzi wa jengo hilo, hivyo mkandarasi anapaswa kuendana na kasi ya ujenzi lakini kwa kuzingatia ubora unaotakiwa.
 

Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, uwepo wa jengo hilo kutauwezesha Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya kujiendesha pamoja na kutumika kuendesha balozi zingine katika maeneo mbalimbali kwa kutumia kitega uchumi hicho.
 
Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu na kukamilika baada ya muda wa miaka mitatu.