Makamu wa Rais Dkt. Mpango aomba nguvu ya (UNEP)

0
188

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira Inger Anderson.

Dkt. Mpango amelishukuru shirika hilo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali nchini Tanzania yenye lengo la kupambana na uharibifu wa mazingira.

Makamu wa Rais amesema kutokana na changamoto za mazingira bado Tanzania inahitaji msaada wa shirika hilo hasa katika kuwezesha tafiti zitakazotoa njia za kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Aidha amesema kutoka na ukataji miti kwaajili ya nishati, Tanzania inakaribisha teknolojia rafiki pamoja na nishati mbadala nafuu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania pamoja na kulinda mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa (UNEP) Inger Anderson ameipongeza Tanzania katika jitihada zake za uhifadhi wa mazingira pamoja na ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa baraza la kimataifa la mazingira uliofanyika jijini Nairobi.

Inger amesema UNEP imefurahishwa na uwepo wa sera ya Taifa ya mazingira ambayo inalenga kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Inger ameongeza kwamba (UNEP) itaendelea kuunga mkono Tanzania katika juhudi hizo za uhifadhi wa mazingira ikiwemo kupambana na taka za plastiki ambazo zimekua tishio la mazingira duniani.