Rais Magufuli ataka udhibiti mapato ya dhahabu

0
1100

Rais Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Madini kuanzisha vituo vya ukaguzi wa madini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na rekodi ya idadi ya madini yaliyouzwa na kudhibiti mapato yatokanayo na madini.

Hayo ameyasema leo Ikulu jijini Dar Es Salaam baada ya kuwaapisha viongozi mbali mbali aliowateua Januari 8 ambao ni Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Balozi na Katibu Tawala.

Amesema kuwepo kwa vituo hivyo kutasaidia nchi kufahamu kiwango cha madini kinachouzwa nje na ndani ya nchi na kusaidia kutopoteza rekodi ya madini.

“Wizara ya Madini hakikisheni mnaanzisha vituo hivyo vya madini kwani kwa kutokuwepo kwake kunachangia taifa kupoteza fedha nyingi kwa kutojua kiasi gani cha madini kimepatikana na kuuzwa”alisema Rais Magufuli.

Wizara inapaswa kuhakikisha inafanya uchunguzi wa kina kuhusu soko kubwa la dhahabu kwani Tanzania inaonekana kutofaidika na biashara hiyo.

Amesema sheria ya madini iko wazi namna ya kuingia mikataba na watu wakubwa na wafanyabiashara hivyo ametoa wito kwa Wizara ya Madini kuhakikisha inaweka mambo sawa.

Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kupitia Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro kwa juhudi za kukamata dhahabu hivi karibuni mkoani Mwanza.

Amesema juhudi za  askari waaminifu ambao walifanikiwa kuwakamata wenzao nane waliokuwa katika nia ya kutorosha madini hayo zimeonyesha kuwa bado jeshi la polisi lina askari waaminifu na wenye uchungu na nchi yao.

Pia Rais amemtaka waziri mpya wa Madini Doto Biteko kuhakikisha anashughulikia masuala muhimu ili kuhakikisha nchi haipotezi mapato kupitia sekta hiyo ya madini.

Ameitaka Benki Kuu ya Tanzania -BOT kuanzisha utaratibu wa kununua dhahabu na kuhifadhi dhahabu hiyo ili isaidie nchi katika pato la taifa.

Kwa viongozi aliowaapisha, Rais Magufuli amewataka kwenda kufanya  kazi kwa bidii na kuacha ubinafsi utakaosababisha kuzorota kwa maendeleo ya taifa.