Wanawake Ruvuma watumia vyakula vya asili kuwaenzi mashujaa

0
154

Wanawake Mkoa wa Ruvuma wamejitokeza na kulipamba Tamasha la kumbukizi ya Miaka 115 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni linalofanyika Mjini Songea kwa kuandaa vyakula vya asili ya makabila ya Mkoa huo ili kuwakumbusha watanzania umuhimu wa vyakula hivyo.

Akiongea kwenye Tamasha hilo, Mama wa Mila wa Mkoa wa Ruvuma, Zainabu Mangoma amesema, vyakula hivyo vilitumiwa na wazee wao waliopigana vita hivyo na kuwa sehemu ya ushujaa wao ulitokana na kula vyakula vinavyoimarisha afya na nguvu ya miili yao hivyo hawanabudi kuwaenzi.

Mangoma anatoa wito kwa Watanzania wote kuhudhuria Tamasha hilo hasa wakazi wa Mkoa huo ili kujikumbusha mambo muhimu ya mila na desturi ambayo ni muhimu kwa ustawi wa nchi kwa ujumla

Frank Kipanga anaeshiriki katika maadhimisho hayo ameeleza kuwa moja ya kilichomvutia zaidi kwenye ushiriki wa akina mama hao hasa kupitia vyakula vyao vya asili vyenye ladha nzuri na tofauti na alivyozoea kula kila siku.

“Kina mama hawa kwangu wamekuwa walimu wakubwa, vyakula vyao vimenivutia sana, nimekula na sikuhisi kuacha kula maana ni vitamu sana, na huwezi kuamini mboga zingine zimetokana na majani ambayo sisi huwa tunayaona ni dawa za vidonda na chakula cha mifugo” Kipanga

Maadhimisho hayo ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni hufanyika kila mwaka tarehe 22 hadi 27 Februari Mjini Songea kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za Serikali na binafsi, wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma, Machifu wa Makabila mbalimbali wa ndani na nje ya nchi