Naibu waziri wa Kilimo asisitiza utafiti kwenye mazao ya Kilimo

0
211

Utafiti wa ardhi inayoambatana na matumizi ya teknolojia katika Kilimo imetajwa kuwa njia mojawapo itakayowasadia wakulima wadogo kuongeza uzalishaji wa mazao yenye tija.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde wakati wa hafla ya kuzindua kipindi kipya cha Kilimo Kwanza kitakachorushwa kupitia TV E ambapo amebainisha kuwa kipindi hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wakulima kupata elimu mbadala katika masuala ya Kilimo.

Mavunde amesema mataifa yaliyoendelea ni kwa sababu ya kuwekeza kwenye tafiti na teknolojia ya kisasa katika kilimo hivyo serikali itaendelea kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kukifanya kilimo nchini kiwe chenye tija kwa wakulima.

Aidha, amesema Kilimo ndio uti wa mgongo wa kila Mtanzania hivyo serikali imedhamiria kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kujikita kwenye Kilimo kwa ajili ya maisha yao na ustawi wa taifa.

Kwa Upande wake mtayarishaji na mhariri wa kipindi hicho, Scholastica Mazula amesema lengo la kuanzisha kipindi hicho ni kuwafikia wakulima katika mikoa yote hususani wakulima wa pamba na alizeti katika mkoa wa Simiyu

Zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wanategemea mazao ya Kilimo ili kujipatia mkate wao wa kila siku ikiwa ni pamoja na kuujenga uchumi wa nchi kupitia kilimo.