Tuwaenzi Mashujaa kwa kufanya kazi

0
113

Watanzania wametakiwa kuwaenzi mashujaa wa Vita vya Majimaji kwa kukuza uchumi wa Taifa na kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhusu sera ya “Tanzania ya Viwanda” na kukuza utalii Ukanda wa Kusini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wibert Ibuge kwenye ufunguzi rasmi wa Tamasha la kumbukizo ya Miaka 115 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni linalofanyika Mjini Songea Mkoa wa Ruvuma.

Balozi Ibuge amesema kuwa maadhimisho hayo ni chachu ya kuhamasisha wadau na jamii kushiriki katika maendeleo ya nchi hasa Mkoa wa Ruvuma kama hatua muhimu ya kuwaenzi Mashujaa waliopigania utu wa wananchi kwa vitendo.

Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa sehemu ya Maadhimisho hayo itakuwa ni kutembelea eneo la kijiji cha Maposeni kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini, mahali ambapo maji ya Vita vya MajiMaji yalianza kutolewa na Nduna Mkomanile na kuanza kutumiwa na Mashujaa wa Vita vya Maji Maji.

“Kijiji cha Maposeni ni makazi ya Chifu Emmanuel Zulu ambaye ni Chifu wa 5 wa kabila la Wangoni. Chifu, amewaalika Machifu wengine kutoka Mikoa mingine nje ya Ruvuma kama vile Njombe, Iringa, Mbeya, Tabora, Mwanza, Lindi na Mtwara. Huko kutakuwa na sherehe za Ngoni Day” Balozi Ibuge

Katibu Mkuu wa Baraza la Makumbusho Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma Mzee Abasi Chitete amesema wao kama wazee wa Mila wa Mkoa huo wameona ni vyema kuhakikisha watoto na wajukuu zao wanarithi urithi adhimu wa Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utamaduni wao.

Maadhimisho hayo ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni hufanyika kila mwaka Mjini Songea kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za Serikali na binafsi, wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma, Machifu wa Makabila mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.