Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema kuundwa kwa bodi itakayosimamia ithibati ya maudhui ya vyombo vya habari itasaidia kuthibiti makosa yanayofanywa na baadhi ya waandishi hali inayosababisha baadhi ya vyombo kufungiwa kutokana na kosa la mtu mmoja.
Hayo yameelezwa na Meneja Huduma za Utangazaji TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka wakati akijibu swali la mmoja wa wachangiaji katika mkutano wa TCRA na wahariri pamoja na wadau wa vyombo vya habari, kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano nchini.
“Baadhi ya waandishi na watangazaji wamekuwa wakikiuka sheria zinazosimamia maudhui ya utangazaji kwa makusudi hivyo bodi ya kuthibiti wa ithibati ya maudhui kwa watangazaji, itasaidia taasisi kuondokana na changamoto ya kufungiwa kwa sababu ya kosa la mtu mmoja,”-Amesema Kisaka.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlka hiyo Dkt.Jabir Bakari amesema kutokana na Teknolojia inavyokuwa kwa kasi na mambo kubadilika lazima ije na changamoto zake ambazo lazima Mamlaka hiyo ichukue hatua kwa kuwashirikisha wadau wake ili kukidhi mahitaji ya walaji.
Kuhusu suala la baadhi ya watu kufanya makosa ya jinai mtandaoni Mkurugenzi wa leseni na Ufuatiliaji kutoka TCRA John Daffa amesema sheria ziko wazi na kwa yeyote atakayebainika kuhusika kufanya kosa la jinai kwenye mitandao.