Vifo vya mama na mtoto vyapungua Kisarawe

0
227

Uzinduzi wa Jengo la Afya ya mama na mtoto katika Hospitali ya wilaya ya Kisarawe iliyopo Mkoani Pwani, imetajwa kuwa muarobaini wa vifo vya wakinamama wajawazito vinavyotakana na matatizo ya uzazi na umbali mrefu wa kufuata huduma kutoka Vifo 15 mwaka 2017 hadi vifo 3 kufikia Disemba mwaka 2021.

Hayo yameelezwa na Mganga mkuu wa Hospitali hiyo Dkt.Libamba Sobo wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la mama na mtoto lililojengwa kwa msaada wa shirika la Jamuhuri ya watu wa Korea KOFIH.

Aidha Dkt.Sobo amesema msaada unatolewa na wafadhili katika kuboresha miundombinu ya kutolea huduma ya afya na mtoto imesaidia wajawazito zaidi ya elfu moja mia nne ndani ya wilaya hiyo na Mikoa jirani sawa na asilimia 69 kujifungua katika Hospitali hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kisarawe Dkt.Seleman Jafo amewashukuru wadau wa afya likiwemo Shirika la ESO kwakuona umuhimu wa kuwezesha Hospitali hiyo kuboresha miundombinu yake pamoja nakutoa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya milioni mia nne kwa ajili kirahisisha utoaji wa huduma bora kwa Ustawi wa wananchi wa Wilaya hiyo.

Naye Afisa mradi kutoka Shirika la KOFIH Dkt.Nyassatu Mwendwa amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha Watanzania wenye Hali ya chini wanapata huduma ya afya ya uhakika.

Baadhi ya Wananchi wa Wilaya hiyo ambao wamehudhuria hafla hiyo wamesema kuzinduliwa kwa Jengo hilo kutasaidia kupunguza kero iliyokuwa ikiwakumba wajawazito hasa kutembea muda mrefu kufuata huduma sehemu zingine.