Simba yamnyemelea Adebayor wa USGN

0
149

Klabu ya Soka ya Simba ya Tanzania imefanya mazungumzo ya awali na wakala wa mchezaji kinara wa mabao katika kundi D kutoka klabu ya Union Sportive Gendarmerie Nationale (USGN) ya Niger ili kumnasa nyota wa Nigeria anayekipiga na klabu hiyo Victorien Adebayor, (25).

Rais wa Klabu ya Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amewaambia waandishi wa habari Mjini Niamey kuwa baada ya kumfuatilia mchezaji huyo wamegundua kuwa ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anastahili kukipiga na Simba.

Try Again amesema, atamshawishi Rais wa Heshima wa klabu hiyo Mohamed Dewj -MO kuvunja benki ili mchezaji huyo asiende kucheza Denmark na badala yake atue msimbazi

“Anastahili kucheza Simba na siyo Ulaya nitamshauri Rais wa Heshima wa Simba kuvunja benki ili kumnasa nyota huyo raia wa Nigeria” amesema Salim Abdallah

Alipoulizwa kuhusiana na yeye kucheza katika klabu ya Simba Adebayor amesema “Simba ni klabu kubwa na yuko tayari kujiunga nayo kama kila kitu kikikaa sawa”

Mchezaji huyo raia wa Nigeria amefunga mabao 2 katika michezo miwili aliyocheza katika michuano ya kombe la shirikisho ambapo klabu yao ya US Gendarmerie inaburuta mkia kwa kuwa na alama moja pekee huku Simba wakiwa vinara wa kundi hilo kwa kujikusanyia alama nne baada ya kucheza michezo miwili.