CCM yapuliza kipenga uchaguzi wa Naibu Spika

0
242

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeanza mchakato wa kupata mgombea atakaye peperusha bendera yake katika uchaguzi wa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania unaotarajiwa kufanyika Februari 11 mwaka huu.

Nafasi hiyo ipo wazi kufuatia Dkt. Tulia Ackson kujiuzulu Januari 31 mwaka huu ili kukidhi vigezo vya kugombea nafasi ya Spika wa Bunge ambayo alishinda katika uchaguzi wa Februari Mosi.

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM, zoezi la kuchukua na kurejesha fomu limeanza Februari 4 na litakoma Februari 6, na litafuatiwa na zoezi la kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya CCM Taifa litakalofanyika Februari 7.

Februari 8 utafanyika mchujo na uteuzi wa mwisho wa wagombea, zoezi litakalofanywa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Mchakato utahitimishwa Februari 10 ambapo Kamati ya Wabunge wa CCM itapiga kura kumpata mgombea wa chama hicho.

Ibara ya 85(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki kwa kila chama cha siasa chenye uwakilishi bungeni kushiri uchaguzi wa kujaza nafasi ya Naibu Spika.