Tulia aweka rekodi uchaguzi wa Spika

0
169

Mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Tulia Ackson ameweka rekodi baada ya kuchaguliwa kwa asilimia 100 na wabunge wote waliopiga kura leo.

Dkt. Tulia ambaye ni Mbunge wa Mbeya Mjini amepata kura 376 kati ya kura 376 zilizopigwa, na kuwaacha washindani wake wengine bila kupata kura yoyote.

Kuchaguliwa kwake kumemfanya kuwa Spika wa Saba wa Bunge la Tanzania, ambapo pia amekuwa spika wa pili mwanamke baada ya Anne Makinda.

Baada ya kuapishwa, amewashukuru wote waliompigia kura na kuahidi kwamba bunge atakaloliongoza litasimamia kikamilifu serikali kwa kukosoa, na kuirekebisha ili kuhakikisha wao kama wabunge wanatimiza msingi wa mhimili huo wa kuwa daraja kati ya wananchi na serikali.

Miongoni mwa shukrani zake amezielekeza kwa Spika Mstaafu, Job Ndugai kwa namna alivyomshauri na kumkuza kama mbunge na nafasi yake ya Naibu Spika aliyoitumikia kwa miaka sita.

Amewaambia wabunge kwamba moja ya dira watakayoitumia katika utekelezaji wa majukumu yao ni hotuba aliyoitoa Rais Samia Suluhu bungeni Aprili mwaka 2021, ambayo inatoa mwelekeo wa nchi na mambo yanayotakiwa kufanyika.

Uchaguzi wa Spika umefanyika leo ukihusha wagombea tisa kutoka vyama mbalimbali, ambapo mbali na Dkt. Tulia, wengine ni Abdullah Mohammed Said (NRA), Mhandisi Aivan Jackson Maganza (TLP), David Daud Mwaijojele (CCK), Georges Gabriel Bussungu (ADA -TEA), Kunje Ngombale Mwiru (SAU), Maimuna Said Kassim (ADC), Ndonge Said Ndonge (AAFP) na Sadoun Abrahamani Khatib (DP).

Wakizungumza baada ya matokeo kutangazwa Ngonde na Maimuna wamesema wamepokea kwa mikono miwili matokeo ya kushindwa kwao, na kwamba watajaribu tena wakati mwingine kwani lengo lao ni kuwatumikia Watanzania.