TANESCO kufanya matengenezo ya mitambo yake

0
121

Katika jitihada za kuboresha upatikanaji wa umeme nchini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linaendelea na maboresho kwenye vituo vyake vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I itakayozalisha megawati 185 na Ubungo III megawati 112.

Akizungumza na wanahabari mapema leo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Maharage Chande amesema mpaka sasa uzalishaji kutoka mitambo ya Ubungo III umefikia Megawati 60 ambazo tayari zimeunganishwa kwenye gridi ya Taifa.

Amesema, kwa sasa kazi ya kupanua kituo cha Kinyerezi I inaendelea na megawati 70 za awali zitaingia kwenye mfumo wa gridi mwezi Aprili 2022 na ifikapo mwezi Agosti 2022 kazi hiyo itakuwa imekamilika na kupelekea Kituo cha Kinyerezi I ambacho sasa kinazalisha megawati 150 kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 335.

‘‘Mitambo hii inayoongezwa ili iweze kuzalisha umeme, inapelekea mahitaji ya gesi asilia kuongezeka ambapo inalazimu kufanya uboreshaji wa mfumo wa gesi kwenye mifumo ya TPDC (Shirika la maendeleo ya Petroli Tanzania) na PAET (Pan African Energy Tanzania),’’ amesema Maharage.

Aliongeza kuwa zoezi la uboreshaji litafanyika kwenye visima vya gesi vilivyopo Songosongo kuanzia tarehe 01 hadi 10 Februari 2022, ambapo kukamilika kwake kutahakikisha gesi ya ziada inayohitajika inapatikana.

Chande amesema utekelezaji wa maboresho hayo utapelekea mapungufu ya gesi kwenye mitambo ya kuzalishia umeme wa gesi asilia na kulazimika kuzimwa kwa baadhi ya mitambo ili kupisha zoezi hilo muhimu.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo maeneo kadhaa yanayopata umeme kutoka katika gridi ya Taifa yataathirika na kutakuwa na mgao wa umeme.