Waziri Ndalichako afanya ziara Ofisi za ATE

0
145

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako akiambatana na Naibu Waziri katika Wizara hiyo Patrobas Katambi mapema leo Jumanne tarehe 25 Januari 2022 wametembelea katika Ofisi za Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Dar es Salaam kwa mazungumzo na utambulisho.

Waziri Ndalichako amefanya mazungumzo na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya ATE ikiongozwa na Mwenyekiti Jayne Nyimbo pamoja na Menejimenti ya ATE ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu Suzanne Ndomba- Doran.

Katika hotuba yake Waziri ameipongeza ATE kama mdau wa UTATU kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiutoa kwa Wizara hiyo katika kuboresha Sekta ya ajira na kazi nchini na kuwasisitiza waajiri wote nchini ambao bado hawajajiunga na ATE kufanya hivyo ili kufaidika na huduma za ATE.

Katika salamu zake Suzanne Ndomba amemshukuru Waziri na ujumbe wake kwa kutembelea Chama cha Waajiri katika siku zake za awali katika Wizara hiyo lakini pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuigawanya Wizara na kuitenganisha na Sera, Bunge na Uratibu kwani italeta wepesi wa kiutendaji katika masuala ya kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.