Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameongoza waombolezaji katika mazishi ya kaka wa Makamu wa Rais na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dkt. Gerald Mpango, yaliofanyika Kasulu Mkoani Kigoma.
Askofu Mpango alifariki dunia tarehe 19 Januari 2022 jijini Dar es salaam.
Ibada ya Mazishi imefanyika katika kanisa la Anglikana la Mtakatifu Andrea Kasulu mkoani Kigoma ikiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Maimbo Mndolwa.
Akizungumza wakati wa mahubiri Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Donald Mtetemela amemtaja Askofu Mpango kama kiongozi aliyempenda Mungu, amesema alikuwa na moyo wa uinjilisti na alihubiri ndani na nje ya nchi na mara zote aliongoza ujenzi wa Makanisa ili kuendelea kuhubiri injili.
Akitoa neno la shukruani kwa niaba ya familia Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msaada wa rambirambi pamoja na neno la faraja katika kipindi cha msiba huo. Makamu wa Rais amesema anashukuru kwa faraja aliopata kutoka viongozi mbalimbali kutoka serikalini pamoja na wastaafu, kutoka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, viongozi wa dini pamoja na taasisi mbalimbali.