Waziri Ndaki atoa maelekezo kwa wakusanya maduhuli

0
166

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ametoa maelekezo manne kwa wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwa lengo la kuhakikisha wanafikia lengo lililowekwa.

Waziri Ndaki ametoa maelekezo hayo kwenye kikao na wataalam wa mifugo kilichofanyika mkoni Dodoma ambapo amewaeleza kuwa mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli ya serikali sio mzuri kwani kati ya bilioni 50 zilizokusudiwa kukusanywa ni bilioni 13.9 ndio zimekusanywa.

Baada ya majadiliano ya taarifa zilizokuwa zimewasilishwa, Waziri Ndaki amewaeleza wataalamu hao kuwa ni lazima wajipange vizuri kuhakikisha wanafikia malengo ya ukusanyaji maduhuli ya serikali kama walivyo pangiwa na kwamba viongozi wataendelea kuwafuatilia.

Wataalam hao pia wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanatimizwa.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo, Tixon Nzunda amewataka wataalam hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu lakini pia watalazimika kuwajibika kutokana na matendo yao kwenye suala la ukusanyaji wa mapato.