Ndejembi akoshwa na wanufaika wa TASA

0
156

Serikali imewataka Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) nchini kuanzisha vikundi vinavyotokana na kaya maskini ili viweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 ambayo imekua ikitolewa na Halmashauri zote nchini kwa Wanawake, Vijana na Walemavu.

Agizo hilo limetolewa Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi wa kilimo cha Mahindi, Karanga na Maharagwe unaotekelezwa na wanufaika wa TASAF katika Kijiji cha Lusaka.

Akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Sumbawanga pamoja na wanufaika hao wa TASAF, Ndejembi amekipongeza kikundi hicho cha akina Mama kwa namna ambavyo wamejiongeza kwa kuanzisha na kusajili kikundi kingine nje ya TASAF na kupata mkopo wa Halmashauri.

“Nimefurahishwa sana na kikundi hiki cha akina Mama, hiki ndicho ambacho Serikali ya Rais Samia inataka kuona. Tunahitaji kuona wanufaika wa TASAF wakitumia vizuri pesa tunazowapatia katika kufanya miradi ya kimaendeleo ili kukuza uchumi wao, niwapongeze Mama zangu kwa kuanzisha kikundi kingine nje ya TASAF na kujipatia mikopo inayotolewa na Halmashauri, huu ni ubunifu mkubwa sana,” amesema Naibu Waziri Ndejembi.