Aliyekuwa Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amewataka wafanyakazi wa TANAPA kuendeleza umoja, mshikamano na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya shirika.
Ametoa wito huo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kwa Kamishna wa Uhifadhi mpya William Mwakilema. Amesema “Mafanikio yaliyofikiwa kwa upande wa TANAPA yanahitaji kulindwa na kuendelezwa kwa kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na kuimarisha mshikamano.”
Ameelekeza TANAPA kuongeza bidii katika kuyatekeleza majukumu ya msingi ambayo ni kuendeleza uhifadhi na utalii. Ametahadharisha kuwepo kwa dalili za ujangili katika hifadhi za Taifa na kusisitiza kuongezwa kwa ulinzi wa maliasili kwa kwa nguvu zote.
Kuhusu utalii, amesisitiza kuongeza bidii ili kuwavutia watalii wa ndani na nje na ili kufikia lengo hilo ni lazima kuboresha miundombinu, kutoa huduma bora kwa watalii na kuendelea kuvitangaza vivutio vyetu.
Naye Kamishna wa Uhifadhi, William Mwakilema ametoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kushika nafasi hiyo na kuahidi kutekeleza kazi kwa dhati na bila upendeleo, chuki wala majungu.