Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi tarehe 17 Januari, 2022 ametembelea Banda la Tanzania katika Maonesho ya EXPO 2020 Dubai yanayoendelea katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE)
Rais Mwinyi ambaye yupo katika ziara ya Kiserikali nchini humo ametembelea banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo Dubai2020 kwa ajili ya kujionea jinsi Tanzania inavyotumia fursa ya Maonesho hayo ya Makubwa Duniani kutangaza Biashara na Uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na Uchumi wa Bluu, Utalii, Madini, Nishati na Kilimo.
Rais Mwinyi amepongeza ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo ikiwa ni miongoni mwa Nchi 192 zinazoshiriki katika Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 1 Oktoba , 2021 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 31 Machi, 2022 ambapo, Ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo unaratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade)
Pia Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi ametembelea Kituo cha Polisi cha mtandao “ Smart Police Station “ kwenye Maonesho hayo ambapo alipewa maelezo kuhusu kifaa maalum kinachotumika kuwasilisha kesi kwa njia ya mtandao.
Katika ziara hiyo, Rais Dk. Mwinyi amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi pamoja na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.