Mradi wa maji Kigamboni kukamilika Aprili 2022

0
117

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imesema mradi wa maji Kigamboni wenye lengo la kutatua changamoto ya maji kwa wananchi utakamilika Aprili mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cpyrian Luhemeja alipotembelea na kukagua mradi huo katika siku ya tatu ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya majisafi na usafi wa mazingira.

“Tulikubaliana na mkandarasi kukamilisha ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni 15 ifikapo mwishoni mwa Januari 2022, na maendeleo yake sio mabaya na mwisho wa Januari tunategemea kukamilisha,” amesema Mhandisi Luhemeja.

Mhandisi Luhemeja amempongeza mkandarasi anayetoa maji visimani kwa kukamilisha ununuzi wa pampu tatu za kusukuma maji, huku akimuagiza kuongeza kasi katika mchakato wa manunuzi ya pampu za kutoa maji visimani kupeleka kwenye tenki.

“Namuagiza mkandarasi kukamilisha manunuzi hayo mapema ifikapo mwezi wa pili mwaka huu ili kukamilisha mradi huu, endapo ifikapo mwezi wa nne mkandarasi hajamaliza mradi tutamwondoa,” amesisitiza Mhandisi Luhemeja.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Luhemeja ameeleza hatua ya pili ya mradi ni kupeleka maji Kongowe kwani ni karibu na maji yapo ya kutosha huku hatua ya tatu itahusisha kupeleka maji Mbagala ambapo yote haya yatafanyika ndani ya mwaka huu kabla ya Disemba.

Shughuli ya usambazaji wa mabomba kupitia mradi huu wa maji Kigamboni inatarajiwa kuanza Jumatatu tarehe 17 Januari mwaka huu huku Afisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Luhemeja akielekeza Menejimenti ya DAWASA kuhakikisha wanaendeleza mapambano kukamilisha mradi huu ndani ya muda.