Shahidi wa tisa kwa upande wa jamhuri, Gladys Fimbari amemaliza kutoa ushahidi wake kwenye kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashitaka ya ugaidi namba 16 ya 2021 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Shahidi huyo ambaye ni Afisa Meneja Kitengo Cha Sheria katika Kampuni ya Airtel Tanzania amekamilisha sehemu ya pili ya ushahidi wake baada ya kuhojiwa na mawakili wa upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili Robert Kidando huku Upande wa Utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala.
Katika sehemu ya pili ya ushahidi wake shahidi huyo amedai barua ya kuombwa taarifa za laini tatu za simu zilizotakiwa kufanyiwa uchunguzi na Jeshi la Polisi kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi amedai zilipelekwa Julai 2, 2021 na kujibiwa siku hiyo hiyo na hakujulishwa iwapo uchunguzi huo ulikuwa juu ya nani.
Shahidi huyo amedai pamoja na kwamba mteja ni mtu muhimu sana kwenye kampuni yao lakini pale ambapo sheria itawataka kutoa ushirikiano kwa taasisi za kiuchunguzi juu ya jambo fulani linalohitaji, itawalazimu kufanya hivyo.
Kuhusu namba inayodaiwa kuwa ni ya mshitakiwa Freeman Mbowe lakini kwa sasa jina linasoma la mtu mwingine, shahidi huyo amesema pale ambapo laini ya simu hiyo haitatumika ndani ya miezi mitatu inafungwa au kupewa mtu mwingine.
Wakati Wakili John Malya akiendelea kuhoji maswali kwa shahidi, Jaji Joachim Tiganga alitoa angalizo kwa wakili huyo kutotoka nje ya mada wakati wa kumuhoji shahidi ili kuepusha hali ya sintofahamu kwa shahidi katika kujibu maswali yanayompasa kujibu.
Baada ya shahidi kukamilisha kutoa ushahidi wake, mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, mwaka 2022 kwa ajili mahakama kuendelea kupokea ushahidi kwa shahidi atakayefuata kwa upande wa jamhuri.