Mwanasheria wa Airtel atoa ushahidi kesi ya Mbowe na wenzake

0
163

Mwanasheria wa Kampuni ya Airtel Tanzania ambaye ni Meneja katika kitengo cha sheria Gladys Fimbari amepanda kizimbani katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutoa ushahidi wake kwenye kesi Uhujumu Uchumi yenye mashataka ya ugaidi namba 16 ya 2021 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Shahidi huyo ambaye ni wa tisa kwenye kesi hiyo kwa upande wa jamhuri ameanza kutoa ushahidi wake juu ya shauri hilo akiwa anaongozwa na wakili wa Serikali Jenitreza Kitali mbele Jaji Joachim Tiganga wa mahakama hiyo.

Akitoa ushahidi wake kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Fimbari amesema akiwa kama mwanasheria wa Kampuni ya Airtel anawajibu wa kutoa ushauri kwenye kampuni juu ya mambo mbalimbali ya kisheria, ikiwemo ufuatiliaji wa kesi za kampuni.

Pia amesema yeye kama afisa meneja wa kitengo sheria ambaye amepata mafunzo ya ziada juu ya mfumo wa mawasiliano ana wajibu wa kutoa ushirikiano kwa taasisi za kichunguzi ikiwemo TAKUKURU, TCRA, taasisi ya kupambana na madawa ya kulevya pale kampuni itakapohitajika.

Amedai Julai 2, 2021 akiwa ofisi za Airtel zilizopo Morocco mkoani Dar es Salaam akiwa anatekeleza majukumu yake Mkuu wake wa idara ya sheria alimpatia barua ili atoe taarifa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Kisayansi juu ya miamala ya fedha pamoja na usajili wa namba tatu za airtel.

Katika maelezo yake shahidi huyo amedai taarifa zilizoombwa na Jeshi la Polisi kitengo cha uchunguzi wa Kisayansi ni zile za kuanzia Juni Mosi, hadi Julai 31, 2021 ambapo amedai baada ya kuingia kwenye mfumo alipata taarifa za usajili wa namba hizo zikiwa zimesajiliwa kwa jina la Freeman Aikael Mbowe ambaye ni mshtakiwa wa nne kwenye kesi hiyo kisha akaandika barua ambayo aliisaini kujibu maombi ya Jeshi la Polisi.

Baada ya maelezo hayo ya awali shahidi huyo ameiomba mahakama ipokee vilelezo vitatu ambavyo ni barua viwe sehemu ya ushahidi wake ambavyo hata upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala umeridhia vipokelewe na mahakama.

Kwa mujibu wa taarifa ya miamala fedha iliyotajwa kwenye vielelezo hivyo vitatu shahidi huyo amedai zilitumwa kwa washitakiwa Mohamed Ling’wenya, Hassan Bwire na Denis Urio ambaye sio mshtakiwa kwenye shauri hilo.