Tuzo za Grammy mwaka 2022 zaahirishwa

0
4844

Hafla ya 64 ya utoaji wa Tuzo za Grammy ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika Januari 31 mwaka huu nchini Marekani imeahirishwa kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO19), waandaaji wameeleza.

Taarifa ya waandaji hao imesema kuendelea kusambaa kwa kasi kwa kirusi aina ya Omicron kumewafanya kuona kuendelea na halfa hiyo kutakuwa na hatari kubwa za kiafya kwa waandaaji na washiriki.

Tuzo hizo ambazo ni moja ya fahari kubwa katika tasnia ya muziki na burudani zitatolewa katika tarehe nyingine itakayotangazwa baadaye.

“Usalama wa kiafya wa familia ya muziki, washiriki wetu, na mamia ya wafanyakazi wetu ni jambo la msingi zaidi kwetu,” Recording Academy na CBS wameeleza.

Mwaka 2021 tuzo hizo ziliahirishwa kutoka Januari 31 hadi Machi 14 zikihusisha njia ya ushiriki wa moja kwa moja na kupitia mtandaoni baada ya kuenea kwa maambukizi ya UVIKO19 huko Los Angeles na California.