Wafugaji washauriwa kufuga kibiashara

0
115

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewashauri Wafugaji nchini kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji wa kuchunga, ambao tija yake imekuwa ndogo kwao na kwa Taifa.

Waziri Ndaki ametoa ushauri huo mkoani Iringa, alipotembelea shamba la kisasa la mifugo la Shaffer.

Akiwa katika shamba hilo kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali Waziri Ndaki amesema, Wafugaji wanatakiwa kuanza kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kiasili ambao umeanza kupitwa na wakati.

“Tumekuwa hatuoni faida kwa mifugo yetu kwa sababu ya kung’a ng’ania ufugaji wa kiasili, wafugaji tuanze kufuga kibiashara ili tuongeze tija ya mifugo yetu.” amesema Waziri Ndaki

Ameongeza kuwa ili Wafugaji waanze kuona tija ya ufugaji wao ni lazima wabadilike na waache ufugaji wa kuzunguka kutafuta maeneo ya malisho, na badala yake wawe na maeneo yao ya kufugia ambayo yatakuwa rahisi kufikiwa na wataalam kwa ajili ya kuwapatia huduma zinazohitajika kwa mifugo yao.

Kwa upande wake msimamizi wa shamba hilo la kisasa la mifugo la Shaffer, Mahboob Malick amesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapatia na kwamba wako tayari kuendelea kushirikiana nayo kwa lengo la kuboresha ufugaji hapa nchini.