Waziri Mkuu wa Sudan ajiuzulu

0
174

Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok ametangaza kujiuzulu wadhifa huo baada ya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum, ya kupinga makubaliano ya kuongoza Serikali ya Mpito.

Hamdok amejiuzulu wadhifa huo zikiwa zimepita wiki chache tangu aliporejea madarakani, baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba mwaka 2021.

Ametangaza uamuzi huo kupitia televisheni ya Taifa ya Sudan, huku akisema anaachia wadhifa huo ili kuruhusu mtu mwingine kusaidia Taifa hilo kuvuka katika kipindi cha mpito cha kuelekea utawala wa kidemokrasia,

Hamdok ametoa wito wa kufanyika kwa majadiliano, ili kufikiwa kwa makubaliano mapya kuhusu namna utawala mpya wa kidemokrasia utakavyoongoza Taifa hilo.

Jeshi la Sudan lilifanya mapinduzi Oktoba 25 mwaka 2021 yaliyoipindua Serikali ya Hamdok, lakini baadaye alirejea kuongoza Serikali mwezi Novemba mwaka huohuo wa 2021.