Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza amekabidhi mitaji ya biashara, mitungi ya gesi 66, pikipiki moja na kompyuta moja kwa kinamama wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania, Wilaya ya Ukerewe lengo ikiwa ni kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Masanja amekabidhi vitu hivyo leo alipotembelea ofisi za Umoja wa Wanawake Tanzania, Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.
“Nimekuja na mtaji wa shilingi laki moja moja kwa kila mwanamke, fedha hizi sasa zikasaidie kuongeza vipato vyenu kwa kufanya biashara ndogondogo” Masanja amefafanua.
Kuhusu mitungi ya gesi , Masanja amesema lengo ni kuwasaidia kinamama hao kutumia nishati mbadala na kuachana na matumizi ya kuni ambazo ni chanzo cha uharibifu wa mazingira.
“Nimekuja na nishati mbadala ambayo itasaidia kinamama hawa kuondokana na changamoto za kutafuta kuni na kwa wakati huo huo watakuwa wanatunza mazingira”amesema Masanja.
Aidha, Masanja amesema pikipiki aliyoikabidhi itumike kuongeza mapato ya umoja huo ili waweze kukua kiuchumi na pia kompyuta hiyo itumike katika shughuli za kiofisi za Umoja huo.